Kim Jong-nam aliuawa kwa kemikali inayoshambulia mfumo wa fahamu

KIM Jong Nam, kaka wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini aliuawa kwa sumu kali iliyopigwa marufuku, taarifa ya serikali ya Malaysia imeeleza.
Kim alifariki wiki iliyopita baada ya wanawake wawili ‘kumshambulia’ katika eneo la ukaguzi kwenye Uwanja wa Ndege wa Kuala Lumpur.
Taarifa ya uchunguzi wa awali nchini Malaysia kuhusu tukio hilo inabainisha kwamba sumu iliyotumika kumdhuru na hatimaye kifo chake ilikuwa aina ya "VX nerve agent,” ambayo Umoja wa Mataifa imeiweka katika kundi la ‘silaha’ za maangamizi.
Hata hivyo, ingawa inaamini Korea Kaskazini ndio imeendesha mpango wa mauaji ya Kim, lakini bado Malaysia haijaihusisha rasmi nchi hiyo iliyopo katika mzozo wa muda mrefu na baadhi ya mataifa ya Magharibi, ikiwamo Marekani.
Kim alifariki dunia akiwa njiani kuwahishwa hospitali baada ya tukio hilo la Februari 13. Mwili wake bado umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali moja nchini Malaysia kutokana na kile kinachotajwa kuwa ni mgogoro wa kidiplomasia juu ya nani anapaswa kuuchukua mwili huo kwa ajili ya shughuli za maziko.
Korea Kaskazini ilitoa majibu ya hasira dhidi ya Malaysia ikisisitiza kufanya uchunguzi wa mwili huo wa Kim, ikisisitiza kuwa Malaysia imekuwa na ‘nia mbaya’ kuhusu tukio hilo
Kuhusu kemikali ya VX nerve agent
Ni silaha kali zaidi ya kikemikali, inayofanana na mafuta na isiyo na ladha wala harufu yoyote- Hufanya kazi kwa kupenya katika ngozi na kushambulia mishipa ya fahamu – tone moja tu kwenye ngozi linaweza kumuua mtu ndani ya dakika chache. Kiasi kidogo kinaweza kusababisha maumivu ya macho, kushindwa kuona vizuri, kizunguzungu na kutapika.
- Inaweza kutumika katika mfumo wa mvuke au kuwekwa kwenye maji, chakula na mazao ya kilimo.
- VX inaweza kuingia mwilini kwa njia ya hewa, kula, kugusa ngozi, au macho.
- Nguo inaweza kukaa na VX kwa muda wa dakika 30 baada ya kupatwa na mvuke wake na inaweza kuwaathiri watu wengine.
- Jina lake la kisayansi ni S-2 Diisoprophylaminoethyl methylphosphonothiolate na imepigwa marufuku katika makubaliano ya mwaka 1993 ya silaha za kikemikali.
Mkuu wa polisi nchini Malaysia Khalid Abu Bakar anasema uwepo wa kemikali hiyo uligundulika katika macho ya marehemu Kim. Kwa mujibu wa Bakar, ushahidi mwingine ulikuwa unafanyiwa uchunguzi zaidi na kwamba polisi walikuwa wanafanya uchunguzi wa namna kemikali hiyo iliyopigwa marufuku ilivyoingia nchini Malaysia.
“Kama kiasi cha kemikali kilichoingizwa kilikuwa ni kidogo, itakuwa ni vigumu kwetu kufahamu,” alinukuliwa na shirika la habari la Reuters.
Bruce Bennet, mtaalamu wa masuala ya silaha katika Taasisi ya Rand Corporation, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kuwa kingehitajika kiasi kidogo sana cha kemikali hiyo kuweza kumuua Kim.

Korea Kaskazini haijamtambua mtu aliyefariki kama Kim Jong Nam, bali kama raia wa Korea Kaskazini.
Kiasi kidogo sana cha kemikali inawezaka kilitumika, alisema Bennett, ambacho kilianza kuathiri mfumo wake wa fahamu mara moja, kusababisha aanze kutetemeka na baadaye kufariki baada ya dakika chache.
Wanawake wawili walionekana katika kamera wakimkaribia Kim, mmoja akipuliza kitu fulani katika uso wake.
Khalid aliwahi kusema kwamba kutokana na mwanamke huyo kwenda kunawa mikono ilionyesha dhahiri kuwa alikuwa anafahamu alikuwa amebeba sumu.
Raia kadhaa wa Korea Kaskazini wanatafutwa kutokana na kuhusika na kifo hicho, akiwemo afisa mmoja wa ngazi za juu katika ubalozi wa Korea Kaskazini huko Kuala Lumpur, pamoja na mfanyakazi wa Shirika la Ndege la Air Koryo.
Kim aliwahi kuonekana kama mrithi wa madaraka kutoka kwa baba yake, Kim Jong Il, lakini haikuwa hivyo na badala yake mdogo wake ndiye akarithi, Kim Jong-un ndiye akarithi madaraka na kaka yake huyo kwa muda mrefu amekuwa akiishi ugenini na amekuwa akisafiri kwa kutumia pasi ya kusafiria yenye jina la Kim Chol. Korea Kaskazini bado haijathibitisha iwapo aliyefariki ni Kim Jong Nam.
Katika taarifa ya kwanza ya Shirika la Habari la Korea Kaskazini kuhusu kifo hicho, serikali ilieleza kwamba Malaysia pekee ndiyo inahusika na kifo cha mmoja wa raia wake.
Pia iliishutumu Malaysia kwa kujaribu kutumia siasa katika suala la kurudisha mwili huo Korea Kaskazini na kuyaita madai ya kupatiwa vinasaba vya ndugu wa karibu wa Kim kama ni ya kipuuzi.

Comments
Post a Comment