Miaka 20 jela kwa kufanya mapenzi na binti yake


MKAZI wa Kijiji cha Kiwanja katika Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya, Maneno Pesambili Kanjanja amehukumiwa kifungo cha miaka 20 jela na viboko vinane kwa kosa la kuzinga na marimu.
Kosa la kuzinga na marimu, kisheria, ni pale watu wenye uhusiano wa damu wanapofanya tendo la kujamiana, kwa lugha ya Kiingereza hufahamika kama “incest.” 
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Chunya, Desdery Aloys Magezi, alimkuta Kanjanja na hatia ya kutenda kosa hilo kwa binti yake wa miaka 19 ambaye wana uhusiano wa damu, kosa ambalo ni kinyume na kifungu Na. 158 (1) (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu, sura Na.16 ya mwaka 2002.
Kwa mujibu wa sheria hiyo, mtu anayekutwa na hatia ya kutenda kosa hilo kwa mwanamke wa chini ya umri wa miaka 18, hukabiliwa na kifungo cha miaka 30 wakati yule anayetenda kwa mwanamke mwenye umri zaidi ya miaka 18 hukabiliwa na kifungo cha miaka 20.
Kanjanja aliangukia kwenye kundi la kutembea na mwanamke (binti yake) mwenye umri wa miaka 19, ni zaidi ya miaka 18 hivyo kuhukumiwa kifungo cha miaka 20.
Katika hukumu yake, Hakimu Mkazi, Magezi alisema pamoja na kifungo hicho cha miaka 20, Kanjanja ambaye pia hufahamika kwa majina ya Maneno Pesambili Lyimo, atachapwa viboko vinane wakati wa kuingia gerezani.
Mbali ya kumwingilia kimwili binti yake, Kanjanja pia alidaiwa kumfungia ndani kwa miaka miwili, kumyima haki za msingi ikiwemo chakula na kumsababishia ulemavu wa miguu kiasi cha kushindwa kutembea.
Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Rehema Madusa alichukua hatua za haraka kulifuatilia na kuhakikisha mtuhumiwa huyo anafikishwa mahakamani akishitakiwa kwa kosa la kumwingilia binti yake kimwili tofauti na awali ambapo polisi waliandika kosa kuwa ni kutohudumia familia.
Mbali ya kumfikisha mahakamani mzazi huyo, mkuu huyo wa wilaya alisimamia uchunguzi wa kiafya wa binti huyo katika Hospitali ya Rufaa Mbeya.

Comments

Popular posts from this blog

MWANJALE AONGEZEWA SIKU NYINGIZE ZA MATIBABU