Msuva aitesa Simba wamzungumzia kila saa!!
Unguja. Taarifa za mshambuliaji wa Yanga, Donaldo Ngoma kutocheza mechi dhidi Simba zimeshtua kidogo, lakini hofu zaidi ya vinara hao wa Ligi Kuu ni Simon Msuva.
Msuva mwenye uwezo wa kucheza winga zote mbili, lakini kocha George Lwandamina anapenda kumtumia zaidi kulia akiwa pamoja na beki Juma Abdul katika kuanzisha mashambulizi.
Kocha wa Simba, Mcameroon Joseph Omog aliposikia Ngoma hachezi alitaharuki na kuuliza na Tambwe (Amissi), lakini akasisitiza kati ya wote, Msuva ndiyo msumbufu.
"Tunacheza na timu nzima, hatuangalii ubora wa mchezaji mmoja mmoja, kama Ngoma hayupo tutakwenda kupambana na yeyote atakayekuwepo,"alisema Omog kocha mwenye uzoefu na soka la Afrika baada ya kufundisha Cameroon, Congo na sasa Tanzania.
Alipoulizwa mchezaji gani Yanga anahitaji uangalizi zaidi, Omog alisema: "Yule anayecheza kama Ngassa nani vile (anajaribu kukumbuka na kisha kutaja) Msuva."
"Ni mchezaji makini ana kasi, nguvu na uamuzi wa haraka pale anapotaka kufanya jambo lake anahakikisha linafanikiwa, hata hivyo wao ni wao, ninachoangalia ni timu yangu namna ya kuiboresha kuhakikisha inanifanyia kazi ninayoihitaji," anasema Omog.
Mbali na kauli ya Omog hata wachezaji na watu wengine wa Simba wanapozungumza kuhusu Yanga jina la Msuva ndiyo linalotajwa.
"Nguvu ya Yanga ipo upande wa kulia anakocheza, Msuva na Abdul ndiyo watu wabaya kama tutafanikiwa kuuzibiti upande huo, tunamaliza kila kitu, pale katikati wanacheza, lakini kule pembeni ndiyo kwenye shida," anasema kiongozi huyo.
Simba ipo Zanzibar ikijiandaa na mechi ya Ligi Kuu dhidi ya Yanga itakayochezwa Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Comments
Post a Comment