Jumuiya ya Afrika Mashariki yakabiliwa na ukata

                                  BLOG NO 1 TANZANIA !!


JUMUIYA ya Afrika ya Mashariki (EAC) inakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa fedha kiasi cha kushindwa kutekeleza majukumu yake muhimu kutokana na nchi wanachama  kushindwa kutimiza wajibu wao wa kuchangia shughuli za Jumuiya hiyo.
Hali hiyo pia imesababishwa na hatua ya baadhi ya nchi wafadhili ambao pia hujulikana kama ‘wabia wa maendeleo’ kukataa ama kupunguza kwa kiasi kikubwa utoaji wa misaada yao,hali inayohusishwa na migogoro ya kisiasa inayoendelea kuzikumba nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Taarifa za ndani ya sekretarieti ya Jumuiya hiyo jijini hapa inasema kuwa michango ya nchi wanachama katika bajeti ya mwaka wa fedha 2016/17 imekuwa ikisuasua huku Uganda tu ndiyo inayoonekana kuchangia zaidi.
Hadi kufikia sasa, kwa mujibu wa taarifa hizo,walau Uganda pekee ndiyo imechangia asilimia 89.39 ya mchango wake wa bajeti ya mwaka 2016/17.
Tanzania ambayo ndiyo Mwenyekiti wa Jumuiya kwa sasa, imechangia asilimia 30.47 huku Kenya, nchi yenye uchumi mkubwa kuliko zote katika EAC, ikiwa imetoa asilimia 52.47 tu ya mchango wake.
Rwanda hadi sasa imetoa asilimia 47.74 ya mchango wakati Burundi ambayo ni nchi masikini kuliko zote katika Jumuiya huku ikikabiliwa na vikwazo kutokana na mgogoro wa kisiasa,hesabu za mchango wake bado hazijajulikana mpaka sasa.
Nchi nyingine mwanachama, Sudan Kusini nayo haijatoa chochote kutokana na kukabiliwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo imesababisha vifo vya maelfu ya wananchi wake huku mamilioni wengine wakikabiliwa na ukosefu wa chakula.
Mgogoro unaochangia EAC kunyimwa fedha na wahisani ni ule wa kisiasa nchini Burundi uliosababishwa na hatua ya Rais Pierre Nkurunziza kuongeza muhula wa tatu wa uongozi wake huku akipingwa vikali nchini kwake na kusababisha mauaji ya kisiasa na maelfu ya wananchi kuikimbia nchi yao.
Hata hivyo, msimamo huo wa Rais Nkurunziza uliungwa mkono na EAC hatua iliyosababisha wafadhili wakubwa wa Jumuiya hiyo, nchi za Umoja wa Ulaya(EU), kupunguza ama kukataa kabisa kuipa misaada EAC.
Akizungumzia suala hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari  juzi, Katibu Mkuu wa EAC Balozi Liberatus Mfumukeko hakutaka kukiri wala kukataa Jumuiya kuwa na hali mbaya kifedha lakini alimwagiza Meneja Uhusiano wa jumuiya hiyo Richard Owora kutoa ufafanuzi wa jambo hilo.
“Hakujakauka kabisa,pamoja na hayo mnayosema, kazi zetu zinaendelea lakini ufafanuzi zaidi mtapata kutoka kwa  Owora baada ya kuwasiliana na  watu wetu wa fedha,” alisema Mfumukeko ambaye ni raia wa Burundi.
Hata hivyo,Owora alielezea kwa ufupi jinsi nchi wanachama zilivyotoa michango yao katika mwaka wa fedha wa 2016/17 huku akisema kuwa nchi hizo ndizo zinazopaswa kutoa fedha za bajeti ya Jumuiya.
“Nchi ya Uganda imefikia asilimia 89.39 katika kutoa mchango wake wa kuiwezesha Jumuiya ijiendeshe ikifuatiwa na Kenya 52.47 %, Rwanda 47.74% ,Tanzania 30.47% “.
“Kuhusu Burundi kwa sasa sina hesabu yake kamili kwani juzi tu ndio waliwasilisha kiasi cha fedha kama mchango wao lakini sio fedha nyingi . Sudan Kusini wao bado , suala la wafadhili kama wametoa au hawajatoa tuliache kwa sababu Jumuiya ni mtoto  wa nchi wanachama, ni jukumu lao kumtunza mtoto huyu na sio kutegemea wafadhili” alisisitiza Owora.
Hali hiyo ya ukata inatarajiwa kuwa moja ya ajenda muhimu katika kikao cha wakuu wan chi wanachama wa Jumuiya kilichopangwa kufanyika Aprili 6 mwaka huu Jijini Arusha.

Comments

Popular posts from this blog

MWANJALE AONGEZEWA SIKU NYINGIZE ZA MATIBABU